Sintofahamu! Jumapili iliyopita kwenye mahubiri ya ibada ya Kanisa la
Ufufuo na Uzima, Mchungaji Kiongozi, Josephat Gwajima alitoa madai
mazito sana kwamba, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Paul
Makonda (36) anatumia cheti cha kidato cha nne cha mtu anayeitwa Paul
Christian Muyenge wakati yeye alianza darasa la kwanza mwaka 1988,
akitumia jina la Daudi Albert Bushite.
AMCHAMBUA KWA VYUO
NI JINA LA MAHAKAMANI?
NANI ANAINGIA?
MKANGANYIKO WA GWAJIMA, PAUL CHRISTIAN
HOTUBA YA MAGUFULI KUHUSU VYETI FEKI
UFUMBUZI NI UPI?
FAIDA ZA MAKONDA KUTOBOA UKWELI
IJUMAA NA VIONGOZI
MEYA WA KINONDONI
PROFESA SEMBOJA
TUMEFIKAJE HAPA?
Akihubiri huku waumini wake wakimsikiliza kwa umakini mkubwa, Mchungaji
Gwajima alisema kuwa, mwaka 2001, Makonda alitumia cheti cha mwanafunzi
huyo chenye divisheni 3 ya ponti 25 ili aweze kujiunga na Chuo cha Uvuvi
Nyegezi (NFTI).
AMCHAMBUA KWA VYUO
Alisema kuwa, alisoma masomo ya certificate na kuhitimu mwaka 2002
ambapo mwaka huohuo, akiendelea kutumia jina la Paul Christian Muyenge,
alijiunga na Chuo Cha Uvuvi Mbegani, Bagamoyo mkoani Pwani kwa masomo ya
Diploma ya Uvuvi (ODMF, NTA LEV. 6) na kuhitimu mwaka 2005.
Gwajima alizidi kusema kuwa, mwaka 2006, Makonda alipata udahili Chuo
cha Ushirika na Biashara, Moshi (wakati huo kikiwa Chuo Kikuu Kishiriki
cha SUA) akiendelea kutumia vyeti vyake vya certificate ya Nyegezi na
diploma ya Mbegani na akijulikana kama Paul Christian Muyenge.
NI JINA LA MAHAKAMANI?
Mchungaji Gwajima alizidi kudai kuwa, jina la Paul C. Makonda,
analitumia baada ya kula kiapo mahakamani kubadili jina na kwa hiyo,
cheti cha kidato cha nne cha mheshimiwa kinasomeka, Paul C. Muyenge
lakini vyeti vya elimu ya juu vinasomeka Paul C. Makonda baada ya kuapa
mahakamani.
Kwa mujibu wa maelezo ya Gwajima, ana maana jina la Daudi lilikufa rasmi kwenye makahama na kuanza kuchipuka kwa jina la Paul.
NANI ANAINGIA?
Kwa mujibu wa Mchungaji Gwajima, mwanafunzi aliyeuza cheti hicho (Paul
Christian Muyenge) anaingia kwenye kashfa ya kuuza cheti kama kweli mtu
huyo yupo na ndiye mwanafunzi halali aliyekuwa akilitumia jina hilo
mpaka mwaka 2001.
MKANGANYIKO WA GWAJIMA, PAUL CHRISTIAN
Wakati Gwajima akidai kuwa na nakala za vyeti vyote viwili vya Paul
Makonda, vikiwemo vile alivyotumia kuanzia kidato cha nne, upo
mkanganyiko mkubwa kutokana na maelezo ya Paul Christian (mtu aliyedaiwa
kumpa vyeti Makonda) aliyoyatoa kwa gazeti moja la kila siku la hapa
nchini.
Paul Christian, anayedaiwa kuwa ndiye ambaye cheti chake kilitumiwa na Paul Makonda aliliambia gazeti hilo;
“Paul Makonda nimemfahamu kupitia habari na jina wanavyolitaja
(waliotunga taarifa ya mtandaoni) wanakosea kwani mimi naitwa Paul
Pierre Christian Kagezi, hatuna uhusiano, mimi Mhaya yeye Msukuma.”
“Taarifa hizo (za kumpa cheti Makonda) si za kweli kwa sababu huwezi
kutoa cheti wakati umepata daraja la kwanza kidato cha sita, utakwenda
vipi chuo kikuu? Sasa niliwezaje mimi kwenda chuo kikuu halafu kwa
wakati huo nimpe naye aende chuo kikuu?”Alihoji.
Cristian aliendelea kudai kuwa katika kidato cha tano na sita, alichukua
mchepuo wa sayansi masomo ya Fizikia, Kemia na Hesabu (PCM), hivyo si
rahisi kutoa cheti hicho kwani angeshindwa kumudu huko alikokwenda.
Alihoji kama Makonda hakufanya vema kidato cha nne au hakusoma kidato
cha sita, akatumia cheti cha mtu mwingine, angeweza vipi kufanya vema
katika mitihani yake ya chuo kikuu?
Alifafanua kuwa watu wamekuwa wakipika na kuoanisha majina yao, huku akiendelea kukanusha kuhusu taarifa hizo.
“Kama wanataka kumpata huyo bwanamdogo (Makonda) kwa njia hiyo
wamemkosa, kwani kwa mantiki nimekuuliza ukipata daraja la kwanza kidato
cha sita lazima uende chuo kikuu?” alihoji.
“Huyo bwana anajitegemea yeye kama yeye na walichokifanya wao
(waliosambaza taarifa mtandaoni) kwa makusudi yao bila shaka wana lengo
lao, wao wametaka kuingiza hoja ambazo hazina mashiko.”
MKANGANYIKO (CONFUSSION) MKUBWA
Kufuatia madai hayo ya Gwajima ambayo yalikuwa ndani ya mahubiri yake,
mitandao ya kijamii na mazungumzo ya watu mitaani, sehemu mbalimbali ya
nchi, gumzo kuu likawa ni jina la; ‘Paul Muyenge na Daudi Bashite.’
Baadhi ya watu walionesha kushangaa kwao kama kweli Makonda anatumia
cheti cha mtu mwingine huku akijua kuwa, serikali ya awamu ya tano chini
ya utawala wa Rais John Pombe Magufuli ilitangaza kupambana na
watumishi wenye vyeti vya bandia.
“Hivi inawezekanaje Makonda akaendelea kutumia cheti cha mtu mwingine
wakati mkuu wake wa nchi ni mkali kwenye eneo hilo? Hili jambo si la
kulifumbia macho kirahisi tu, ni jambo zito. Gwajima akae na kujua kuwa,
alitoa tuhuma nzito sana ambazo kama zinathibitika zina ukweli, Makonda
anaweza kung’oka kwenye nafasi yake” alisema Bakar Msumari, mkazi wa
Mbezi Mwisho.
HOTUBA YA MAGUFULI KUHUSU VYETI FEKI
Katika moja ya hotuba zake za kuonesha mwelekeo wa serikali yake, Rais
Magufuli alisema kuwa, atakapogundua, mtumishi yeyote katika serikali
yake anatumia vyeti feki, basi atamfukuza mara moja bila kujali ni nani
(akimaanisha hatajali cheo). Na tangu aanze utawala wake, Magufuli
amekuwa ni mtu anayesimamia kile anachokiongea.
“Ndugu zangu Watanzania katika hili la vyeti wala hawana sababu ya kuwa
na hofu, tunachotaka sisi ni kujua je, huyu mtu anayelipwa kwa sababu
ana masters, kweli ni yake? Kwa sababu kuna watu wanalipwa mishahara
mikubwa kwa sababu ya vyeti vyao ambavyo kiuhalisia siyo vya kwao. Wewe
kama umeishia darasa la saba, usihofu, utaendelea na kazi kama kawaida,”
alisema Magufuli akimaanisha kuwa, hataki watumishi wenye vyeti feki.
Baada ya hotuba hiyo, watumishi wa umma wenye vyeti feki walianza
kusakwa kote nchini, wakiwemo wa Mkoa wa Dar es Salaam na wale ambao
wamebainika, walichukuliwa hatua na zoezi bado linaendelea.
UFUMBUZI NI UPI?
Baadhi ya watu waliamini kuwa, maneno ya Gwajima si jambo la kuwafanya
waamini ni kweli kutokana na historia ya mtumishi huyo wa Mungu ambapo,
amewahi kukwaa kesi mahakamani kufuatia kudaiwa kumtusi Kadinali
Polycarp Pengo katika ibada moja aliyoifanya kwenye kanisa lake (wakati
huo, Kawe).
Wengi walisema kuwa, alichokiongea Gwajima si ukweli kwa asilimia mia
moja, bali mwenye ukweli ni Makonda mwenyewe ambaye wasomaji wanaamini
ndiyo mwenye uwezo wa kuanika ukweli na kufuta madai ya Gwajima na
ufumbuzi wa madai yake kujulikana.
Ijumaa liliweza kuongea na baadhi ya wasomaji ambao walisema kuwa, ni
wakati muafaka kabisa kwa Makonda kuibuka na kuweka wazi au kujibu
tuhuma za Gwajima ili mambo yaishe na maisha yaendelee.
“Gwajima si msemaji wa mheshimiwa Makonda, aliyoyasema si kwamba ndiyo
ukweli. Kwani mara ngapi watu wanaibuka na kujifanya wanawajua wengine
lakini baadaye inabainika kuwa si kweli?” alisema msomaji mmoja
aliyejitambulisha kwa jina la David Mashaka, mkazi wa Salasala, Dar.
“Nilimsikia Gwajima, lakini sijakubaliana naye moja kwa moja. Makonda
ndiye mwenye ukweli wote. Ufumbuzi wake ni kwamba, Makonda ajitokeze na
kuweka wazi anachokijua yeye, siyo mtu mwingine tu amsemee,” alisema
Omar Kishapu, mkazi wa Kimara Suka.
FAIDA ZA MAKONDA KUTOBOA UKWELI
Baadhi ya watu wamesema kuwa, Makonda kujitokeza na kutatua fumbo hilo
kutaleta faida kwani atakuwa ameilinda serikali yake ya awamu ya tano
lakini pia atakuwa amemsaidia Rais Magufuli katika kukitimiza kile
anachokisimamia kama rais wa nchi.
“Inawezekana Makonda kuendelea kukaa kimya kukawapa watu neno la kumsema
rais kwamba mbona hamchukulii hatua. Lakini kumbe hamchukulii hatua kwa
sababu anaujua ukweli, lakini je wananchi wanaujua ukweli? Si mpaka
Makonda mwenyewe auseme, akiuanika ukweli itampa heshima Magufuli na
yeye mwenyewe pia ataendelea kuheshimika na kuaminika,” alisema Maria
Kaparasule, mkazi wa Boko, Dar.
IJUMAA NA VIONGOZI
Juzi, Ijumaa liliwatafuta baadhi ya viongozi ili wazungumzie madai ya
Gwajima ambapo, awali Msemaji wa Tume ya Maadili ya Watumishi wa Umma,
Honoratus Ishengoma alisema:
“Mimi kwanza kabisa nipo likizo. Lakini madai ya Gwajima kusema ule
ukweli ni mazito sana. Hayo madai yanatakiwa kusemewa na Mkurugenzi wa
Tume ya Maadili.”
Ijumaa lilimpigia simu, bosi wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma lakini hakupatikana hewani mara moja.
MEYA WA KINONDONI
Ijumaa lilimpigia simu, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta
ambaye Gwajima alimtaja kuwa rafiki kipenzi wa Makonda lakini simu yake
iliita muda mrefu bila kupokelewa hata iliporudiwa tena na tena.
PROFESA SEMBOJA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Haji Semboja yeye alipoulizwa kuhusu madai ya Gwajima alisema:
“Kosa la Makonda ni kutaja majina ya watu na kuwatuhumu kufanya hivi
wakati hawajathibitika, sasa na sisi hatupaswi kurudia makosa hayo ya
kumtaja kwa jambo ambalo hatuna uhakika nalo. Ni jukumu lenu nyinyi kama
waandishi wa habari kuchimbua na kuja na majibu, je, vyeti hivyo ni
feki au la.
“Hapa kuna hoja mbili, ya kuwa na vyeti feki au kutumia jina la mtu
katika masomo yake. Mimi ni mtu mzima, wakati wetu, lilikuwa ni jambo la
kawaida mtu kusomea jina la mtu mwingine, ambaye alishindwa kuendelea
na masoma kwa sababu mbalimbali. Kama alisomea jina la mtu mwingine,
lakini masomo alisoma yeye, sioni kama kuna tatizo, ila kama elimu
aliyonayo hajawahi kuipata darasani, hilo ndilo tatizo.
“Mimi nadhani tujikite katika kumsaidia rais kwenye mambo magumu
anayofanya, kwa sababu ndiye rais anayesimamia vitu kikamilifu,
tusimchoshe kwa vitu vidogovidogo, kwangu mimi Makonda ni mchapakazi,
huenda ndiyo maana anakutana na vigingi, lakini kwa kweli siwezi kusema
lolote hadi ithibitike kosa lake hasa ni lipi.”
TUMEFIKAJE HAPA?
Februari 2 na 9, mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alianza zoezi
la kutangaza majina ya watu wanaojihusisha na madawa ya kulevya ‘unga’
kwa maana ya kuuza au kutumia. Kila aliyemtaja alitakiwa kufika Kituo
Kikuu cha Polisi Dar ‘Sentro’ kwa mahojiano na polisi. Miongoni mwa watu
waliotajwa ni Gwajima.
Gwajima alifika kituoni hapo na kuwekwa ndani kwa siku kadhaa kisha
akaachiwa. Baada ya kuachiwa, alifanya mkutano na waandishi wa habari
akionesha kusikitishwa kwake kwa Makonda kumtaja jina yeye akidai kuwa,
hajawahi kutumia unga wala kuuza.
Kwa hiyo kumtaja kwake kwamba anatumia vyeti feki inaweza kuwa ni katika kutoa hasira au ‘kulipa kisasi’ dhidi ya Makonda.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni