MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kelele zinazoendelea
dhidi yake ni dalili za mafanikio katika vita dhidi ya dawa za kulevya.
Makonda ameyasema hayo jana alipokuwa mgeni rasmi katika tamasha la Twendezetu Kigamboni lililofanyika katika wilaya.
Amesema, mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni ya kufa au kupona.
“Mfahamu kuwa tunapambana kati ya mauti na uzima, kelele, mwangwi
vinavyoendelea sasa ni dalili njema kwamba tunaendelea kunyooka,”
amesema Makonda.
Makonda alisema Dar es Salaam ya sasa anaifananisha na chuma
kilichopinda na sasa kiko katika hatua ya kunyooka hivyo lazima zitokee
kelele nyingi kama ambavyo zinaendelea sasa.
“Huwezi kufanya kazi ya kunyoosha chuma bila kusikia mwangi, kelele na
maumivu kwa sababu kazi ya kukomboa vijana dhidi ya dawa za kulevya si
rahisi,” amesema Makonda.
Amesema katika kipindi hicho ambacho amekiita kuwa ni cha kulinyoosha
Jiji la Dar es Salaam ni lazima kelele zisikike, uonekane moto unaoacha
maumivu makali na baada ya hapo ije picha ya chuma kilichonyooka ambayo
ndio picha ya Jiji la Dar es Salaam itakayokuwa imenyooka.
Amesema kelele hizo zitapita na mwisho lazima kufika ng’ambo ya pili
pasipo na dawa za kulevya, kwenye taifa lililojengwa na uchumi imara.
Amelipongeza Jeshi la Polisi kwa jitihada zake za kuhakikisha dawa za
kulevya zinatokomezwa ambapo alisema hivi sasa katika Jiji la Dar es
Salaam dawa hizo zimepungua.
“Nitoe pongezi kwa Jeshi la Polisi dawa za kulevya zimepungua sasa Dar
es Salaam na pia niwapongeze pia vijana ambao wanaendelea kutoa
taarifa,” alisema Makonda.
Aliwaasa wananchi kushirikiana na Rais John Magufuli ambaye anafanya
jitihada kuijenga Tanzania ya kesho iliyo bora. Kuhusu Kigamboni alisema
anatarajia kuiona Kigamboni ikiwa mji wa mfano ambao haujaharibiwa na
matendo yasiyofaa ikiwa ni pamoja na uhalifu na vijana walioharibika
kutokana na matumizi ya dawa za kulevya badala yake kuwe na vijana
wachapakazi.
“Watu watakapokuja Kigamboni wakute ni mji msafi, salama, uliopangika
unaofaa kupumzika… mji ulio salama usio na uhalifu,” amesema Makonda.
Amewataka wakazi wa wilaya hiyo kushirikiana na Mkuu wa Wilaya hiyo,
Hashim Mgandilwa na viongozi wake katika kutimiza ndoto hiyo ya kuifanya
Kigamboni tulivu na salama.
Amewaasa wazazi kuhakikisha wanafuatilia mienendo ya watoto wao
kuhakikisha hawajiingizi katika matumizi ya dawa za kulevya na pia
vijana kuchungana wao wenyewe.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Mgandilwa alisema lengo la tamasha hilo ni
kuzitambulisha fursa zilizopo katika wilaya hiyo, kuwakutanisha vijana
kupiga vita dawa za kulevya na pia kuiunga mkono serikali katika kufanya
mazoezi.
Tamasha hilolilihudhuriwa pia na Mbunge wa Jimbo hilo, Dk Faustine
Ndungulile Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Rahel Mhando na Katibu Tawala
wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni