AMIRI Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Dk. John Magufuli amefanya mabadiliko madogo ya utendaji ndani ya Jeshi la Polisi kwa kumhamisha Kamishina wa Operesheni na Mafunzo, CP Paul Chagonja.
Habari
za uhakika zilizopatikana mjini Dar es Salaam jana, zinasema Rais
Magufuli amemteua Kamishina Chagonja kuwa Kamishina mpya wa Jeshi la
Zimamoto na Uokoaji.
“Rais
amefanya mabadiliko madogo ndani ya Jeshi la Polisi, amemhamisha
Kamishina Chagonja tangu jana (juzi) kwenda Zimamoto…nadhani ni
mabadiliko ya kawaida tu.
“Kama
unavyojua Rais Magufuli anakwenda na falsafa yake ya ‘Hapa Kazi Tu’
inaonekana amedhamiria kuboresha maeneo yote…huwezi kujua leo wizara hii
kesho wizara nyingine, tunapaswa kujiandaa kila kukicha ndugu yangu,”kilisema chanzo chetu cha habari.
Kamishina
Chagonja, amekuwa katika nafasi hiyo kwa muda mrefu tangu utawala wa
aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) mstaafu Said Mwema.
“Chagonja
ametumikia nafasi hii muda mrefu kidogo kuanzia wakati ule wa IGP Mwema
mpaka sasa IGP Mangu (Ernest), naamini kutokana na uzoefu wake
imeonekana anafaa kwenda huko,”kilisema chanzo hicho.
Kamishina
Chagonja katika utumishi wake, amewahi kuwa Mkufunzi Mkuu wa Chuo cha
Polisi Moshi na baadae Mkuu wa Chuo cha Polisi Dar es Salaam.
Januari
22, 2013, Rais mstaafu Jakaya Kikwete alimteua Pius Makuru Nyambacha
kuwa Kamishina Jenerali wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji.
Hivi sasa nafasi hiyo inakaimiwa na Kamishina Jenerali Rogatius Kipali.
Alipotafutwa msemaji wa kikosi hicho, Puyo Nzalayaimisi simu yake ya kiganjani iliita bila kupokelewa.
Hata
hivyo Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba alipotafutwa
kuzungumzia mabadiliko hakuweza kupatikana kutokana na simu yake kuita
bila bila kupokewa.
Januari
mwaka huu bungeni mjini Dodoma, aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini,
Godbless Lema (Chadema), alimshambulia kwa maneno makali Kamishna
Chagonja, kwa kumtuhumu kuwa anaweza kuwa anashirikiana na majambazi
wanaovamia vituo vya polisi na kupora silaha.
Lema
alitoa maneno hayo makali, wakati akichangia taarifa za Kamati za Bunge
za Hesabu za Serikali Kuu (PAC) na Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali za Mitaa (LAAC).
Akichangia
hoja hizo, Lema aliliambia Bunge kuwa Chagonja anaweza kuwa anahusika
katika matukio ya ujambazi katika vituo vya polisi kwa sababu anataka
kudhoofisha utendaji kazi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest
Mangu.
Katika
maelezo yake hayo, Lema alilifananisha taifa na chumba kinachotumiwa na
vijana wa kihuni kuishi ambacho hakina utaratibu unaoeleweka wa muda wa
chakula na malazi.
“Mheshimiwa
mwenyekiti, geto ni mahali ambapo watu wanaishi bila kufuata utaratibu,
yaani katika geto, wakati wa kulala anayewahi ndiye anayelala
kitandani. Geto chakula kinapopikwa kinaweza kuliwa hata kama hakijaiva,
kwa hiyo nchi hii naifananisha na geto kwa sababu watu wanaiba fedha za
umma kama wanavyotaka.
“Katika
ripoti za Bunge zilizosomwa hapa jana (juzi) zimejaa wizi, kila ukurasa
wa taarifa ya Zitto (aliyekuwa mwenyekiti wa PAC) ni wizi tu, wizi tu,
hivi huu wizi utakwisha lini? Hata zile bunduki zinazoibwa katika vituo
vya polisi zinaweza kuwa ni ‘sabotage’ (hujuma), zinazofanywa na
Chagonja dhidi ya IGP,” alisema Lema.
Alisema
amefanya uchunguzi wake binafsi uliobaini kuwa Jeshi la Polisi
limegawanyika na kwamba haamini kama Rais Jakaya Kikwete (mstaafu)
amekwishafanya mabadiliko ya uongozi ndani ya jeshi hilo.
Chanzo: Mtanzania
Chanzo: Mtanzania
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni