Uteuzi wa Salma Kikwete kuwa mbunge wa kuteuliwa na Rais umeibua mjadala
katika viunga mbalimbali nchini kutokana na ukweli kwamba hilo
halikuwahi kutokea katika historia ya Tanzania, lakini kimataifa si
jambo geni hata kidogo.
Kwa mara ya kwanza tangu Uhuru, Rais John Magufuli alimteua Mama Salma
ambaye ni mke wa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kuwa mbunge akiwa
mteuliwa wa tisa kati ya nafasi 10 za kufanya hivyo kwa mujibu wa Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Mama Salma ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM,
anaungana na wake wengine wa marais duniani kuingia kwenye nafasi za
uongozi na siasa.
Hillary Clinton
Mwingine ni Hillary Clinton, mke wa Rais wa zamani wa Marekani, Bill
Clinton. Mama huyo ameweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa
na Demoratic kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu
uliofanyika hivi karibuni Marekani kabla ya kushindwa kwa Donald Trump,
ambaye ni Rais.
Miaka minane iliyopita, Hillary alishindwa na Barack Obama katika mchujo
wa kumpata mgombea urais wa chama hicho lakini baada ya Obama kuwa
Rais, alimteua kuwa Waziri wa Mambo ya Nje mwanzoni mwa mwaka 2009. Mama
huyo pia aliwahi kuwa Seneta wa New York mwaka 2000.
Graça Machel
Katika orodha hiyo pia yumo Graça Machel. Huyu ni mwanamke wa kwanza
duniani kuwa ‘first lady’ wa marais wawili tofauti. Alikuwa mke wa Rais
wa Msumbiji, Samora Machel kuanzia mwaka 1975 hadi 1986 na mke wa Rais
wa Afrika Kusini, Nelson Mandela tangu 1998 hadi 2013.
Aliteuliwa kuwa waziri wa elimu na utamaduni wa Msumbiji mara baada ya
nchi hiyo kupata uhuru na mwaka huohuo akaolewa na Rais Samora.
Winnie Mandela
Aliyewahi kuwa mke wa Rais wa Afrika Kusini, Winnie Mandela ni kati ya
wake za marais wanaoingia kwenye historia ya kuwa wanasiasa na viongozi.
Winnie licha ya kushiriki bega kwa bega katika harakati za ukombozi wa
nchi hiyo pia amewahi kushika nafasi mbalimbali za kiuongozi serikalini
na pia katika chama tawala nchini humo, ANC akiongoza wanawake.
Rosario Murillo
Nchini Nicaragua, Rais Daniel Ortega aliishangaza dunia aliposhinda
nafasi hiyo kwa mara ya nne na mkewe aliyekuwa mgombea mwenza kuwa
Makamu wa Rais. Rais Ortega alishinda uchaguzi huo kwa asilimia 72.5 na
kuandika historia katika siasa za dunia ya nchi kuongozwa kidemokrasia
na mume na mke.
Suala hilo liliipa shida nchi hiyo kujua ataitwa jina gani? Ni First Lady yaani mke wa rais au makamu wa rais.
Janeth Museveni
Miongoni mwao ni Janet Museveni ambaye mumewe, Rais Yoweri Museveni wa
Uganda alimteua kuwa waziri wa elimu na michezo katika baraza lake lenye
mawaziri na manaibu waziri 80.
Awali, Mama Janeth alikuwa waziri wa masuala ya eneo la Karamoja lililo
Kaskazini – Mashariki mwa Uganda ambalo lilikuwa limegubikwa na migogoro
na umaskini uliokithiri.
Wasemavyo wachambuzi
Akizungumzia uteuzi wa Mama Salma, Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM), Benson Bana alisema kuwa mke wa Rais hakumzuii mtu
kuteuliwa katika nafasi nyingine ya uongozi ikiwa anazo sifa stahiki.
Alisema hakuna cheo kinachoitwa ‘first lady’ kwenye Katiba na kwamba
kilichomfanya ateuliwe ni utendaji wake mzuri aliouonyesha hasa kuguswa
na matatizo ya wananchi jambo linalomuongezea sifa ya ziada ya kuwa
msemaji wao bungeni.
“Alimsaidia vizuri Rais Kikwete wakati akiwa madarakani. Rais Magufuli amezingatia vigezo, ni haki yake kikatiba,” alisema.
Mratibu wa Taifa wa Taasisi ya wanawake Ulingo, Dk Ave Maria Semakafu
alisema, “Amekuwa kwenye siasa muda mrefu sasa, kwahiyo sioni tatizo
lolote katika uteuzi huo tunachopigania ni kuongeza nguvu zaidi katika
uwakilishi ndani ya Bunge ili kufanikisha hoja za uongozi.”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni